Huduma ya jamii

Samhällsservice – swahili

Kwenye ukurasa huu, unaweza kusoma maelezo kuhusu huduma za kawaida zaidi za umma nchini Uswidi, kama vile shule, matibabu na matunzo ya jamii.

Muhtasari

  • Watu wanaoishi nchini Uswidi wanapata vizuri huduma za jamii.
  • Wakimbizi wanaohamia nchi nyingine hupokea msaada kutoka kwa mashirika mbalimbali.
  • Watoto hupewa nafasi ya kujiunga na shule ya chekechea kuanzia umri wa mwaka mmoja.
  • Kwa watoto wenye umri wa kati ya miaka 6 na 16, ni lazima waende shuleni na bila malipo.
  • Shule ya chekechea ya wazi inapatikana kwa wazazi kuitembelea na watoto wao.
  • Huduma za afya zinapatikana kwa kila mtu, lakini unaweza kungoja kwa muda mrefu.
  • Afya ya akili ni suala muhimu nchini Uswidi. Inakubalika kuzungumzia au kutafuta matibabu ikiwa mtu anahisi kuwa na tatizo la kiakili.
  • Kuna kliniki za wakunga kwa wanawake wajawazito.
  • Nchini Uswidi, ni muhimu kuwa na afya ya mdomo na kutunza meno yako kwa makusudi ya uzuiaji wa magonjwa. Watoto na vijana wanaweza kumwona daktari wa meno bila malipo.
  • Huduma ya ustawi wa jamii husaidia na kutoa msaada kwa watoto, vijana, familia na wazee.
  • Polisi, huduma za dharura na huduma ya usafirishaji wa wagonjwa zinawajibika kwa ulinzi na usalama wa wakazi. Wananchi wanaziamini sana.
  • Piga simu kwa nambari 112 ukiwa katika hali za dharura.

Mashirika ya serikali nchini Uswidi

Nchini Uswidi, utapata mashirika mbalimbali yaliyo na majukumu tofauti katika jamii. Kuna, kwa mfano, mashirika yanayotoa msaada wa fedha ukiwa mgonjwa, unatafuta kazi au umestaafu. Ili jamii iweze kufadhili msaada wa fedha ambao wakazi hupata unapohitajika, kila mtu anayeishi nchini Uswidi lazima alipe ushuru. Kiasi cha ushuru wa kulipa huamuliwa kulingana na kiasi cha mapato yako.

Unaweza kutembelea tovuti za mashirika mbalimbali ili upate maelezo zaidi. Katika tovuti hizo unaweza pia kuona jinsi unavyoweza kuwasiliana na mashirika haya na lugha zinazotumika.

Nembo ya Shirika la Ukusanyaji Ushuru la Uswidi (Skatteverket, Swedish Tax Agency)

Shirika la Ukusa­nyaji Ushuru la Uswidi

Kati ya shughuli kuu za Shirika la Ukusanyaji Ushuru la Uswidi (Skatteverket, Swedish Tax Agency) ni kusimamia usajili wa raia, kusajili anwani na kusimamia ushuru. Utakutana na Shirika la Ukusanyaji Ushuru la Uswidi (Skatteverket, Swedish Tax Agency) unapojisajili, kumaanisha kwamba unasajili data yako ya binafsi na shirika hilo. Kila mtu anayejisajili nchini Uswidi atapokea nambari ya kitambulisho ya kitaifa na anaweza kuomba kadi ya kitambulisho, ambayo ni muhimu, kwa mfano, unapofungua akaunti ya benki au unapotembelea kituo cha huduma za afya.

Ikiwa unaolewa nchini Uswidi, lazima uwasiliane na Shirika la Ukusanyaji Ushuru la Uswidi (Skatteverket, Swedish Tax Agency) mapema kwa ajili ya kufanywa kwa kitu kinachojulikana kama uchunguzi wa vizuizi vya kuoa/kuolewa. Hufanywa ili kuhakikisha kwamba hakuna vizuizi kwa ndoa hiyo, kwamba watu wanaooana wana umri wa zaidi ya miaka 18, si jamaa wa karibu au ikiwa mmoja wao tayari ameoa/kuolewa. Katika Shirika la Ukusanyaji Ushuru la Uswidi (Skatteverket, Swedish Tax Agency), maelezo pia husajiliwa mtoto anapozaliwa au mtu anapokufa.

Shirika la Ukusanyaji Ushuru la Uswidi (Skatteverket, Swedish Tax Agency) lina pia jukumu la kukusanya ushuru unaolipa kwa mapato yako.

Shirika la Ukusanyaji Ushuru la Uswidi (kwa Kiingereza) External link, opens in new window.

Nembo ya Shirika la Huduma ya Umma ya Kuajiri Wafanyakazi (Arbetsförmedlingen, Public Employment Service)

Shirika la Bima ya Jamii la Uswidi (Swedish Social Insu­rance Agency)

Shirika la Bima ya Jamii la Uswidi (Försäkringskassan, Swedish Social Insurance Agency) hushughulikia na kuamua kuhusu aina tofauti za malipo kulingana na hatua uliyofika maishani. Kwa mfano, ikiwa uko katika likizo ya uzazi na unamtunza mtoto mdogo, unaweza kuomba malipo ya "manufaa ya uzazi". Ikiwa wewe ni mgonjwa kwa muda mrefu, unaweza kuomba "manufaa ya ugonjwa". Unaweza pia kuomba msaada na malipo ikiwa una ulemavu. Shirika la Bima ya Jamii la Uswidi (Försäkringskassan, Swedish Social Insurance Agency) linawajibika kwa kusimamia na kulipa msaada wa makaribisho ambao wageni wana haki ya kupokea baada ya kusajiliwa katika mpango wa msaada wa makaribisho.

Wewe mwenyewe una jukumu la kuomba malipo mbalimbali katika Shirika la Bima ya Jamii la Uswidi (Försäkringskassan, Swedish Social Insurance Agency). Ikiwa itatambulika kwamba ulitoa maelezo yasiyo sahihi kwa Shirika la Bima ya Jamii la Uswidi (Försäkringskassan, Swedish Social Insurance Agency) ili kupokea malipo, kumaanisha kwamba umelipwa pesa nyingi zaidi, unaweza kulazimika kurudisha pesa hizo.

Shirika la Bima ya Jamii la Uswidi (kwa Kiingereza) External link, opens in new window.

Huduma ya Umma ya Kuajiri Wafa­ny­a­kazi

Kati ya mambo mengine, Huduma ya Umma ya Kuajiri Wafanyakazi (Arbetsförmedlingen, Public Employment Service) ina jukumu la kuwasaidia wanaotafuta kazi nchini Uswidi. Shirika hili haliwezi kukupa kazi, lakini linaweza kukusaidia kutafuta kazi na kujibu maswali yako kuhusu soko la kazi.

Shirika la Huduma ya Umma ya Kuajiri Wafanyakazi (Arbetsförmedlingen, Public Employment Service) linawajibika kwa mpango wa msaada wa makaribisho unaolenga wageni wanaohamia nchini Uswidi. Ni manispaa ambayo hukusaidia kufanya mawasiliano ya kwanza na shirika la Huduma ya Umma ya Kuajiri Wafanyakazi (Arbetsförmedlingen, Public Employment Service) ili ushiriki katika mpango wa msaada wa makaribisho.

Huduma ya Umma ya Kuajiri Wafanyakazi (kwa Kiingereza) External link, opens in new window.

Matunzo ya watoto na shule ya

Matunzo ya watoto na shule ya chekechea

Kuanzia umri wa mwaka mmoja, watoto wanaweza kuanza shule ya chekechea. Utaomba nafasi kuanzia tarehe ambayo unataka mtoto wako aanze shule ya chekechea. Inafanya iwe rahisi kwa wazazi wote wawili kufanya kazi au kusoma.

Ukuaji wa mtoto huimarika kutokana na kushiriki katika shughuli za shule ya chekechea. Katika shule ya chekechea kuna wafanyakazi wenye ujuzi wanaotimiza mahitaji ya watoto kupitia shughuli za kila siku. Kama mzazi mlezi, unalipa ada ili mtoto wako akae katika shule ya chekechea. Ada ya kulipa inalingana na mapato ya jumla ya familia. Watoto hupewa chakula katika shule ya chekechea.

Shule ya chekechea ya wazi

Shule ya chekechea ya wazi ni mahali pa kukutanika ambapo wazazi au watu wengine wazima wanaweza kukutana na kukaa na watoto, ikiwa hawaendi katika shule ya chekechea. Katika shule ya chekechea ya wazi, unaweza kukutana na wazazi na watoto wengine na hivyo pia kujifunza lugha ya Kiswidi. Kuna wafanyakazi ambao hufanya kazi katika shule za chekechea za wazi na ambao hupanga shughuli zinazofanyika huko, lakini unahusika na unawajibika pia kwa ajili ya mtoto wako. Shule za chekechea za wazi zinapatikana katika manispaa nyingi nchini Uswidi na hazilipishwi.

Mwalimu wa kike na kundi lake la watoto.

Picha: Ann-Sofi Rosenkvist/imagebank.sweden.se

Elimu ya shule ya msingi ya lazima

Watoto huanza madarasa ya shule ya chekechea wakiwa na umri wa miaka sita na huenda shuleni hadi gredi ya tisa. Elimu ya shule ya msingi ni ya lazima nchini Uswidi. Shule za Uswidi hufuata mtaala wa kitaifa, kumaanisha kwamba watoto wote hupata elimu sawa kote nchini. Elimu ya kuanzia shule ya msingi hadi kiwango cha chuo kikuu mara nyingi hailipishwi.

Nchini Uswidi, sare za shule hazitumiki, lakini watoto wanaweza kuvaa nguo zozote wanazopenda kwenda nazo shuleni. Hii pia inajumuisha nguo za kidini kama vile buibui au ishara nyingine za kidini.

Uhusiano kati ya mwalimu na wanafunzi ni muhimu na kazi ya mwalimu ni kuwapa wanafunzi fursa ya kusoma vizuri. Mwalimu huwaelekeza watoto shuleni na kufuatilia jinsi wanavyoendelea. Walimu wana haki ya kuwarekebisha watoto ambao ni wasumbufu. Mwalimu haruhusiwi kuwaadhibu watoto, kwa kuwachapa au kuwadhulumu kisaikolojia.

Mati­babu na afya

Huduma ya afya

Una haki ya kutafuta matibabu katika kituo cha afya. Kituo cha afya kina madaktari na wauguzi ambao wanaweza kukusaidia moja kwa moja au kukuelekeza kwa mtaalamu ikiwa inahitajika.

Ni muhimu uzungumze na mtoa huduma ya afya kuhusu ugonjwa wako au dawa unazotumia ili uweze kupata usaidizi sahihi kwa wakati unaofaa. Wafanyakazi wanaofanya kazi katika sekta ya huduma ya afya wanafuata kanuni ya usiri, kumaanisha kwamba hawawezi kufichua maelezo kuhusu hali yako ya afya kwa mtu mwingine yeyote bila idhini yako. Hii pia inahusu wanafamilia wako.

Una haki ya kupata usaidizi kutoka kwa mkalimani ikiwa huzungumzi Kiswidi, na hutalipishwa chochote. Ukijiumiza au ukiwa mgonjwa sana, una haki ya kutafuta matibabu mara moja katika hospitali iliyo karibu nawe.

Katika mfumo wa huduma ya afya wa Uswidi, unaweza kukutana na wataalamu wa huduma ya afya ambao ni wataalamu wa magonjwa mbalimbali. Hii inaweza kumaanisha kwamba, unapotafuta matibabu, unaweza kulazimika kuweka miadi na madaktari tofauti.

Ubaguzi hauruhusiwi katika huduma ya afya ya Uswidi. Mtu yeyote anayetafuta matibabu lazima apate matibabu.

Huduma ya afya nchini Uswidi ni nzuri, lakini haina wafanyakazi wa kutosha. Hii inamaanisha kwamba unaweza kungoja kwa muda mrefu. Kuna mpangilio fulani unaozingatiwa katika matibabu, kumaanisha kwamba wale wanaohitaji matibabu zaidi ndio watasaidiwa kwanza.

Soma maelezo zaidi kuhusu huduma ya afya ya Uswidi (kwa Kiingereza) External link, opens in new window.

Lango la kuingia katika kituo cha afya.

Picha: Shirika la Uhamiaji la Uswidi (Migrationsverket, The Swedish Migration Agency)/Tomislav Stjepic

Afya ya akili

Nchini Uswidi, afya ya akili inazingatiwa kuwa muhimu zaidi kama afya ya mwili. Kwa hivyo ni muhimu uwe na mazoea ya afya katika maisha yako ya kila siku ili kukuza afya ya akili na mwili. Mifano ya mazoea kama hayo ni kupata usingizi wa kutosha, kula vyakula bora na mbalimbali na kufanya mazoezi.

Kuna usaidizi unaoweza kupata ikiwa unahisi kwamba una matatizo ya kiakili kama vile kushindwa kulala, msongo wa mawazo, wasiwasi, kushikwa na hofu kwa ghafla au huzuni. Mara nyingi unaweza kupata msaada au matibabu katika kituo chako cha afya. Inaweza, kwa mfano, kuhusisha kupata ushauri, msaada wa kimazungumzo au matibabu ya kisaikolojia. Matibabu mengine pia yanapatikana kwa simu au mtandaoni. Unaweza pia kupata matibabu ya dawa. Wakati mwingine unaweza kuelekezwa kwa kliniki ya matibabu ya magonjwa ya akili na daktari katika kituo cha afya, lakini pia unaweza kuwasiliana moja kwa moja na kliniki ya matibabu ya magonjwa ya akili.

Anwani, nambari ya simu na saa za kufunguliwa kwa kliniki mbalimbali (kwa Kiswidi) External link, opens in new window.

Daktari wa kiume na mgonjwa.

Picha: Kristin Lidell/imagebank.sweden.se

Huduma ya uzazi

Kama mjamzito, inapendekezwa utembelee kliniki ya ukunga mara kwa mara ili kuchunguza na kufuatilia maendeleo yako na ya mtoto aliye tumboni. Ni muhimu uwasiliane na kliniki ya ukunga ikiwa wewe ni mjamzito, hata kama ni kwa hiari yako. Hulipishwi kutembelea kliniki ya ukunga.

Kwa kawaida unapaswa kutembelea kliniki angalau mara sita hadi kumi ukiwa mjamzito. Ziara hizo zinaweza kuongezwa ikiwa inahitajika, kulingana na jinsi unavyohisi na jinsi mtoto anavyokuwa tumboni. Wanawake wote wajawazito hufanyiwa uchunguzi wa ultrasound katika ujauzito wao. Ukifika wakati wa kujifungua, una haki ya kuchagua hospitali ambayo ungependa kwenda kujifungulia.

Uchunguzi wa Ultrasound kupitia huduma ya uzazi.

Picha: Simon Paulin/imagebank.sweden.se

Duka la dawa na dawa

Ni maduka ya dawa yanayotoa na kuuza dawa za kuagizwa na daktari nchini Uswidi. Ili uweze kununua na kuchukua dawa fulani, unahitaji agizo la daktari, ambalo kwa kawaida huagizwa na daktari. Muuguzi au mkunga anaweza kuandika agizo la dawa kwa dawa zingine.

Katika duka la dawa, unaweza pia kununua dawa ambazo hazijaagizwa na daktari. Wauzaji dawa ni wataalamu na wamezoea kutoa ushauri kuhusu dawa, lakini ni madaktari ndio walio na wajibu wa kutoa matibabu halisi ya dawa.

Lango la kuingia katika duka la dawa.

Picha: Shirika la Uhamiaji la Uswidi (Migrationsverket, The Swedish Migration Agency)/Björn Bjarnesjö

Matibabu ya meno

Sehemu kubwa ya matibabu ya meno nchini Uswidi ni ya uzuiaji. Hii inamaanisha kwamba mtu hutembelea daktari wa meno mara kwa mara kwa uchunguzi na ufuatiliaji wa afya ya mdomo.

Watoto na vijana wana haki ya kupata matibabu ya meno bila malipo na ikiwa ni pamoja na mwaka ambapo wanafikisha umri wa miaka 23, na wanatakiwa kumtembelea daktari wa meno mara kwa mara. Watu wazima lazima waweke miadi na walipie gharama ya matibabu ya meno. Watu wazima ambao hawana uwezo wa kulipa gharama ya matibabu ya meno wakati mwingine wanaweza kuomba msaada kutoka kwa Shirika la Bima ya Jamii la Uswidi (Försäkringskassan, Swedish Social Insurance Agency), unaojulikana kama msaada wa matibabu ya meno.

Huduma ya ustawi wa jamii

Huduma ya ustawi wa jamii inaweza kusaidia na kutoa msaada kwa watoto, vijana, familia na wazee. Kwa mfano, hutoa huduma ya ushauri kwa familia na mazungumzo ya familia ikiwa unaihitaji. Huduma ya ustawi wa jamii pia hutoa msaada ikiwa wewe au mtu fulani katika familia yako ana tatizo la mazoea ya matumizi ya pombe au dawa za kulevya. Inaweza pia kuwezesha kuwasiliana na makao ya wanawake ya karibu na kutoa msaada wa makao ya muda. Katika huduma ya ustawi wa jamii, unaweza kuomba msaada wa fedha ikiwa huwezi kujitegemea.

Polisi, huduma za dharura na huduma za kusafirisha wagonjwa

Kuna mashirika mbalimbali ya serikali ambao yanawajibika kwa ulinzi na usalama wa wakazi. Polisi, huduma za dharura na wafanyakazi wa huduma ya kusafirisha wagonjwa wana ujuzi na wana jukumu la kusaidia kila mtu anayeishi nchini. Wananchi wanaamini zaidi mashirika haya na wafanyakazi wake. Huduma ya usafirishaji wa wagonjwa nchini Uswidi ina vifaa vya kutosha na inaweza kufikiwa na kila mtu.

Wazimamoto, gari la polisi na gari la wagonjwa.

Wazimamoto, gari la polisi na gari la wagonjwa.

Anwani ya mawasiliano wakati wa dharura

Ikiwa kuna hali ya dharura, lazima upige simu kwa nambari 112. Piga tu simu kwa nambari hii ikiwa kuna hatari ya moja kwa moja kwa maisha, mali au mazingira. Simu hujibiwa na mhudumu wa SOS ambaye jukumu lake ni kuuliza maswali ili kutathmini aina ya msaada unaohitajika katika hali maalum ya dharura. Wahudumu wote wa SOS huzungumza Kiswidi na Kiingereza. Ikiwa inahitajika, mkalimani wa lugha nyingine anaweza kuunganishwa kwenye mazungumzo.

112 – hali za dharura

Piga simu ya dharura kwa nambari 112 kwa hali za dharura kama vile, kwa mfano, ugonjwa wa dharura na matukio ya moto au uhalifu unaofanyika.

Piga tu simu kwa nambari 112 ikiwa kuna hali za dharura. Ikiwa una maswali ambayo si ya dharura, tafadhali tumia moja ya nambari za simu zilizowekwa hapa chini.

1177 – ushauri kuhusu afya na huduma ya afya

Piga simu kwa nambari 1177 ikiwa unahitaji huduma isiyo ya dharura. Utapata majibu ya maswali kuhusu magonjwa na huduma za afya.

114 14 – Polisi katika matukio yasiyo ya dharura

Maswali ya kuzingatia

  • Wananchi wa Uswidi kwa ujumla wanaamini zaidi mashirika ya Uswidi na wafanyakazi wake. Watu katika nchi yako waamini mashirika ya serikali kwa kiwango gani?
  • Je, unajua mtu wa kumwendea ikiwa unahitaji maelezo au kutumia huduma ya umma?

Last updated: