Maelezo ya msingi kuhusu jamii ya Uswidi

Introduktion till det svenska samhället – swahili

Kwenye ukurasa huu unaweza kusoma kuhusu jinsi manispaa yako itakavyokusaidia, jinsi ya kuanza maisha yako nchini Uswidi na msaada wa kujumuishwa katika jamii unaopatikana.

Muhtasari

 • Manispaa ambapo utaishi itakupa msaada wa nyumba na kuanza maisha nchini Uswidi.
 • Ili upate nambari ya kitambulisho ya kitaifa, utahitaji kujiandikisha mwenyewe kama mwananchi wa Uswidi katika Shirika la Ukusanyaji Ushuru la Uswidi (Skatteverket, Swedish Tax Agency). Utahitaji nambari ya kitambulisho cha binafsi cha Uswidi, kati ya vitu vingine, ili uweze kutumia huduma za umma. Kwa hivyo, tafadhali tembelea Shirika la Ukusanyaji Ushuru la Uswidi (Skatteverket, Swedish Tax Agency) mara tu ukiwa na nafasi.
 • Watu wazima, wanaume na wanawake, wenye umri wa miaka 18 hadi 64 hushiriki katika mpango wa makaribisho. Utajifunza lugha ya Kiswidi, kufahamishwa na kutambulishwa katika jamii kabla ya kutafuta kazi nchini Uswidi. Unaweza kushiriki katika mpango huu hadi kipindi cha miaka miwili.
 • Unaposhiriki katika mpango wa makaribisho, unaweza kuomba msaada wa fedha kutoka kwa jimbo ili ukusaidie kulipa gharama zako za maisha.
 • Watoto na vijana huanza kwenda shuleni baada ya kufika na kukaa kwa muda. Ni lazima watoto waende shuleni na ni bila malipo.
 • Ikiwa umefikisha umri wa miaka 65, hushiriki katika mpango wa msaada wa makaribisho, lakini bado unaweza kutafuta kazi. Ikiwa huna ajira, unaweza kutafuta msaada kutoka kwa jimbo ili kulipa gharama za maisha.
 • Lugha ya Kiswidi ni sehemu muhimu ya kujumuishwa kwako katika jamii na kuna njia kadhaa za kujifunza lugha hiyo.
 • Katika kipindi cha mwanzo utashirikiana na watu kadhaa tofauti. Hawa ni wawakilishi kutoka katika manispaa, wasimamizi katika Huduma ya Umma ya Kuajiri Wafanyakazi (Arbetsförmedlingen, Public Employment Service), walimu shuleni na wafanyakazi katika mfumo wa huduma ya afya. Watakutambulisha katika jamii ya Uswidi, kukupa msaada na kujibu maswali yako.

Msaada kutoka kwa manispaa yako

Nchini Uswidi, kuna manispaa 290 na kila manispaa ni sehemu ya eneo maalum la nchi ya Uswidi. Kila manispaa ina shirika ambalo linasimamia na linawajibika kwa, kwa mfano, shule, matunzo ya wazee na msaada kwa familia.

Manispaa ambako umepelekwa itakusaidia katika kuanza maisha yako nchini Uswidi. Manispaa hufanya kazi kwa njia tofauti na msaada ambao yanatoa unaweza kuwa tofauti.

Ni vigumu kusema jinsi hali ya makaribisho yako itakavyokuwa kabisa katika manispaa yako, lakini kwa ujumla manispaa inawajibika kwa

 • kuwa tayari imekuandalia nyumba unapokuja nchini Uswidi.
 • kutoa elimu kwa Kiswidi kwa wahamiaji (SFI, Swedish for Immigrants), kukutambulisha katika jamii na elimu nyingine ya watu wazima.
 • kutoa elimu ya msingi, shule ya chekechea na matunzo ya watoto.
 • kukujulisha kuhusu jinsi ya kujiandikisha kama mwananchi wa Uswidi katika Shirika la Ukusanyaji Ushuru la Uswidi (Skatteverket, Swedish Tax Agency).
 • kukujulisha kuhusu jinsi ya kuweka miadi ya kukutana na Huduma ya Umma ya Kuajiri Wafanyakazi (Arbetsförmedlingen, Public Employmentservice).
 • kukuelekeza katika kuomba msaada wa fedha.
 • kukujulisha kuhusu jinsi ya kuomba huduma ya afya.
 • kuhakikisha unapokea huduma ya ukalimani au kupata huduma ya mkalimani katika huduma za umma. Unapoweka miadi, lazima utujulishe ikiwa unahitaji mkalimani.

Kuji­an­di­kisha kama mwananchi wa Uswidi

Baada ya kufika nchini Uswidi, lazima ujiandikishe kama mwananchi wa Uswidi, katika Shirika la Ukusanyaji Ushuru la Uswidi (Skatteverket, Swedish Tax Agency). Hii inamaanisha kwamba Shirika la Ukusanyaji Ushuru la Uswidi (Skatteverket, Swedish Tax Agency) hurekodi data yako ya binafsi katika sajili yake ya wakazi wa Uswidi. Kujiandikisha ni lazima na ni sharti ili uweze kupata nambari ya kitambulisho ya kitaifa ya Uswidi na kadi ya kitambulisho. Utahitaji nambari ya kitambulisho ya kitaifa na kadi ya kitambulisho ili uweze kufaidika na huduma nyingi za umma.

Baada ya kujiandikisha, inaweza kuchukua muda kabla ya kupata nambari yako ya kitambulisho cha kitaifa na kadi ya kitambulisho. Kwa hivyo ni muhimu ujiandikishe haraka iwezekanavyo.

Soma maelezo zaidi kuhusu kuanza maisha nchini Uswidi (kwa Kiingereza) External link, opens in new window.

Uchunguzi wa afya

Baada ya kufika nchini Uswidi, utaombwa kufanyiwa uchunguzi wa afya, mkalimani akiwepo. Uchunguzi huo si wa lazima na ni wa bila malipo.

Ni muhimu wakati wa uchunguzi ujulishe mfanyakazi kuhusu magonjwa au matatizo yoyote ya afya uliyo nayo, kimwili na kisaikolojia, ili uweze kupata msaada na matibabu unayohitaji. Daktari na mkalimani wanahitajika kisheria kudumisha usiri wa maelezo yote kuhusu afya yako na maelezo yako ya siri. Hii inamaanisha hawapaswi kutoa maelezo hayo kwa mtu mwingine yeyote bila idhini yako, si hata kwa wanafamilia wako.

Ikiwa wewe humeza dawa mara kwa mara, lazima umwambie mtu anayekukaribisha katika manispaa yako au wakati wa uchunguzi wa afya haraka iwezekanavyo, ili uweze kupata dawa unazohitaji. Ili uweze kununua dawa fulani nchini Uswidi, unahitaji uwe umezungumza na daktari kwanza.

Mpango wa maka­ri­bisho wa watu wazima

Watu wazima wote wenye umri wa kati ya miaka 20 na 64 wananufaika na mpango wa msaada wa makaribisho, ambayo mtu hushiriki kupitia Huduma ya Umma ya Kuajiri Wafanyakazi (Arbetsförmedlingen, Public Employment Service).

Mpango wa msaada wa makaribisho una shughuli mbalimbali na lengo lake ni wewe ujifunze Kiswidi haraka iwezekanavyo, utafute kazi na ujitegemee.

Mpango huo unajumuisha kusoma Kiswidi kwa wahamiaji (SFI, Swedish for immigrants), kushiriki katika shughuli ya kutambulishwa kwa jamii na kupokea elimu katika viwango mbalimbali. Unaweza kuhitaji kukuza au kuimarisha ujuzi wako, kuthibitisha msingi wako wa elimu au maarifa ya awali, uwezekano wa kuandikwa kama mwanafunzi na kupokea msaada unapotafuta ajira.

Kwa kawaida unashiriki katika mpango huu wakati wote, kumaanisha siku tano kwa wiki, Jumatatu hadi Ijumaa, kwa saa nane kwa siku. Unaweza kushiriki kwa kikomo cha kipindi cha miaka miwili. Wakimbizi wote wanaohamia nchi nyingine watashiriki katika mpango huo bila kujali jinsia, msingi wa elimu au ajira.

Ikiwa una mtoto mwenye umri wa chini ya mwaka mmoja, huwezi kushiriki kwa sababu unapaswa kukaa nyumbani na mtoto. Mtoto wako akifikisha umri wa mwaka mmoja na anaweza kuanza kwenda katika shule ya chekechea, unaweza kuanza au kuendelea kushiriki katika mpango wa msaada wa makaribisho.

Kuna uwezekano wa kushiriki katika mpango kwa vipindi, kwa mfano kwa sababu ya ugonjwa au ulemavu.

Soma maelezo zaidi kuhusu mpango wa makaribisho (kwa Kiingereza) External link, opens in new window.

Msaada wa fedha

Wakimbizi wengi wanaohamia nchi nyingine huhitaji msaada wa fedha mwanzoni ili waweze kulipa gharama zao za maisha. Lengo ni kwamba hatimaye utaweza kujitegemea na unatarajiwa kutafuta ajira kwa bidii.

Msaada wa kawaida zaidi wa fedha kwa watu wazima kama wakimbizi wageni waliohamia nchi nyingine ni msaada wa makaribisho. Unaweza kupokea msaada huu ikiwa unashiriki katika mpango wa msaada wa makaribisho wa Huduma ya Umma ya Kuajiri Wafanyakazi (Arbetsförmedlingens, Public Employment Service). Ombi la msaada wa fedha hutumwa kwa Shirika la Bima ya Jamii la Uswidi (Försäkringskassan, Swedish Social Insurance Agency). Msaada huu hulipia tu gharama muhimu zaidi kama vile kodi ya nyumba, chakula, miadi ya kumwona daktari na dawa, mavazi kiasi na usafiri wa umma.

Kuna pia aina nyingine za msaada wa fedha nchini Uswidi. Aina ya msaada na kiasi cha msaada unachoweza kupokea inategemea, kwa mfano, iwapo una watoto na gharama ya kodi yako ya nyumba. Malipo ya msaada kwa kawaida hufanyika mara moja kwa mwezi na inahitaji uwe na akaunti ya benki.

Nchini Uswidi, misaada mingi ya fedha hulipwa kandokando kwa kila mtu mzima katika familia. Hii inamaanisha kwamba kila mtu mzima anahitaji kuwa na akaunti yake ya binafsi ya benki na lazima aombe mwenyewe msaada wa fedha. Manispaa inaweza kukuelekeza kuhusu jinsi ya kufungua akaunti ya benki na jinsi ya kuomba misaada mbalimbali ya fedha.

Misaada mbalimbali ya fedha na huduma za jamii zinazopatikana nchini Uswidi zinafadhiliwa kupitia ushuru. Wakazi wote wanaweza kuomba msaada na kwa hivyo kila mtu ana pia jukumu la kulipa ushuru na kujitahidi kuunda mazingira bora kwa ajili yake na jamii kwa ujumla. Kiasi cha ushuru unaolipa ni tofauti kati ya manispaa, lakini kiasi cha wastani cha ushuru ni asilimia 32 ya mapato yako.

Soma maelezo zaidi kuhusu msaada wa makaribisho (kwa Kiingereza) External link, opens in new window.

Soma maelezo zaidi kuhusu na uombe msaada wa makaribisho (kwa Kiswidi) External link, opens in new window.

Matunzo ya watoto na elimu kwa watoto na vijana

Kwenda shuleni ni lazima nchini Uswidi na hii inamaanisha kwamba ni lazima watoto wote waende shuleni kuanzia shule ya chekechea hadi gredi ya 9, ambayo kwa kawaida ni kuanzia umri wa miaka 6 hadi 16. Wengi wao huendeleza elimu yao katika kiwango cha juu cha shule ya upili. Elimu ni ya bure, ikiwa ni pamoja na vitabu vyote vya shule na vifaa vyote muhimu vya shule. Hakuna ada ya kujiandikisha shuleni na hakuna masharti ya sare ya shule.

Watoto na vijana wageni huanza kwenda shuleni baada ya kufika na kukaa kwa muda mfupi nchini Uswidi. Vijana wengi wenye umri wa zaidi ya miaka 16 lakini chini ya umri wa miaka 20 hupewa pia nafasi ya kupata elimu.

Watoto wageni wanapoanza kwenda shuleni, walimu hupima ujuzi wao ili kuamua darasa linalowafaa zaidi katika mfumo wa shule wa Uswidi. Shule hurekodi umri wa mtoto na mara nyingi watoto huwekwa katika darasa la kawaida na wenzao wenye umri unaotoshana sambamba na darasa la maandalizi. Darasa la maandalizi humwandaa mtoto ili aweze kufuata mafunzo ya kawaida. Kiasi cha mafunzo yanayopaswa kutolewa katika darasa la maandalizi na kiasi cha mafunzo yanayopaswa kutolewa katika darasa la kawaida ni tofauti kwa kila mtoto.

Watoto wenye ulemavu au matatizo ya kujifunza wanaweza kupokea usaidizi na msaada wa ziada shuleni.

Mwalimu wa kiume anawafunza watoto katika dawati la shuleni.

Picha: Ann-Sofi Rosenkvist/imagebank.sweden.se

Unachopaswa kujua kuhusu elimu nchini Uswidi:

 • Elimu nchini Uswidi hailipishwi.
 • Hakuna sare ya shule au ada ya kujiandikisha.
 • Watoto hupewa vitabu vya shule na vifaa vingine bila malipo.
 • Wavulana na wasichana hushiriki katika shughuli zote za shuleni pamoja.
 • Watoto wenye umri wa chini ya miaka sita huhudhuria shule ya chekechea, ili wazazi waweze kufanya shughuli mbalimbali.
 • Shule ya chekechea ina gharama inayotegemea mapato ya familia.
 • Chakula ambacho watoto hupewa katika shule ya chekechea na shule ya msingi hakilipishwi.

Nchini Uswidi, wazazi walezi na walezi wana jukumu muhimu katika hali ya watoto kwenda shuleni kwa sababu wanawajibika kuhakikisha kwamba watoto wao wanaenda shuleni hadi na ikiwa ni pamoja na gredi ya tisa.

Mara moja kwa muhula, wazazi walezi na watoto kwa kawaida hufanya mkutano na mwalimu ili kuzungumza kuhusu jinsi mtoto anavyoendelea shuleni. Unaitwa ukaguzi wa matokeo. Kama mzazi mlezi, ni muhimu umsaidie mtoto, kwa mfano, kwa kufuatilia ratiba ya shule ya mtoto na kuhakikisha watoto wanafanya kazi ya shuleni ya kufanyia nyumbani, au kuhakikisha kwamba mtoto anasaidiwa kufanya kazi ya shuleni ikiwa hana muda wakati wa shule au hawezi kuifanya mwenyewe.

Soma maelezo zaidi kwenye tovuti ya Shirika la Kitaifa la Elimu (National Agency for Education) (kwa Kiingereza) External link, opens in new window.

Watoto katika kantini shuleni.

Picha: Susanne Walström/imagebank.sweden.se

Shughuli na msaada kwa watu wazima wenye umri wa zaidi ya miaka 65

Ikiwa umefikisha umri wa miaka 65, hushiriki katika mpango wa msaada wa makaribisho. Ikiwa una zaidi ya umri wa miaka 65, unapokea msaada wa fedha kutoka kwa jimbo. Unaruhusiwa kufanya kazi, hata hivyo, ni faida kwa njia kadhaa. Ajira inaimarisha mapato yako na kukupa nafasi nzuri ya kujishughulisha na kujifunza lugha.

Hata kama hujaariwa, kuna mambo mengine unayoweza kufanya, kama vile kujifunza Kiswidi, kutafuta shughuli unazopenda kufanya na marafiki. Unaweza kuomba manispaa yako maelezo kuhusu shughuli na miungano unayoweza kujiunga nayo.

Wanandoa wazee wameketi mezani pamoja.

Picha: Image bank Sweden

Maneno ya kawaida

Kiarabu

Kiingereza

Kiswidi

Karibu

Welcome

Välkommen

Hujambo

Hello

Hej

Habari zako?

How are you?

Hur mår du?

Nzuri

I am fine

Jag mår bra

Asante

Thank you

Tack

Karibu

You are welcome

Varsågod

Tafadhali

Please

Snälla

Samahani

Sorry

Förlåt

Unaitwaje?

What is your name?

Vad heter du?

Jina langu ni …

My name is …

Jag heter …

Sielewi

I do not understand

Jag förstår inte

Sizungumzi Kiswidi

I do not speak Swedish

Jag pratar inte svenska

Kwaheri

Goodbye

Hej då

Maswali ya kuzingatia

 • Msaada wa fedha utalipia tu gharama za msingi. Unafikiri gharama za msingi inamaanisha nini?
 • Je, maelezo ambayo umesoma kwenye ukurasa huu yamebadilisha matarajio yako uliyokuwa nayo kuhusu msaada utakaopokea?
 • Je, una maoni yoyote kuhusu unachohitaji kufanya ili uweze kujitegemea na kuwa mwanajamii wa Uswidi?

Last updated: