Nyumba

Bostad – swahili

Kwenye ukurasa huu unaweza kusoma kuhusu aina ya nyumba ambazo wakimbizi wanaohamia nchi nyingine hupewa na kinachohusika unapoishi katika nyumba ya kukodisha.

Muhtasari

 • Manispaa yako itakuwa tayari imekuandalia nyumb baada ya kuwasili. Ukikataa nyumba uliyopewa, utahitaji kutafuta nyumba nyingine mwenyewe.
 • Aina za nyumba zinazotolewa zinaweza kuwa tofauti na kutofautiana kwa ukubwa na kiwango.
 • Vifaa vya msingi vinapatikana, yaani, vitu ambavyo vinahitajika kwa kupika, kula, kulala na kuosha. Nyumba imewekwa tu vitu muhimu pekee.
 • Unalipa kodi ya nyumba yako. Unaweza kuomba msaada wa fedha wa kulipa kodi yako ya nyumba.
 • Nyumba za kukodisha zina kanuni ambazo kila mtu anayeishi humo lazima afuate. Hakikisha unapata maelezo kuhusu kanuni za nyumba yako unapoanza kuishi humo.
 • Unahakikishiwa kupata nyumba katika kipindi cha miaka miwili ya kwanza unayoishi nchini Uswidi. Baada ya hapo, unaweza kuhitaji kutafuta nyumba mpya. Ni vigumu kupata nyumba, kwa hivyo jiandikishe katika orodha ya wanaotafuta nyumba haraka iwezekanavyo.

Nyumba za wakimbizi wanaohamia nchi nyingine

Manispaa ya mahali ambapo unahamia hukupangia nyumba katika kipindi cha miaka miwili ya kwanza unayokaa nchini Uswidi. Mara nyingi, utapewa nyumba katika jengo la nyumba za kukodisha, lakini pia unaweza kupewa chumba katika makazi unayoishi na watu wengine au kuishi katika bweni au kambi. Katika hali hizi, utatumia jikoni na bafu na watu wengine, lakini utakuwa na kitanda chako peke yako cha kulala.

Manispaa hujitahidi kuzingatia ukubwa na mahitaji ya familia inapowapangia nyumba wakimbizi wanaohamia nchi nyingine. Wakati mwingine, manispaa hukuruhusu uendelee kuishi hata baada ya miaka miwili kupita. Katika hali nyingine, baada ya miaka hii miwili, unaweza kuhitaji kupanga nyumba nyingine. Kwa sababu ya upungufu wa nyumba za kukodisha nchini Uswidi, ni vyema ikiwa tayari utaanza kufikiria kuhusu kutafuta nyumbani yako mwenyewe baada ya kufika.

Manispaa yako hukupatia chaguo la nyumba moja pekee. Ukikataa nyumba hiyo, utahitaji kutafuta nyumba mwenyewe.

Eneo la makazi lenye nyumba za kukodisha nchini Uswidi.

Picha: Shirika la Uhamiaji la Uswidi (Migrationsverket, The Swedish Migration Agency)/Björn Bjarnesjö

Watoto wanacheza nje ya nyumba za kukodisha.

Picha: Ulf Lundin/imagebank.sweden.se

Kiwango cha nyumba na vifaa

Nyumba za wakimbizi wanaohamia nchi nyingine zinatofautiana kwa aina, ukubwa na kiwango. Nyumba zote zina umeme na maji ya mfereji. Maji ya mfereji ni salama kunywa, kupikia na kuoshea. Nyumba zote zimefunikwa na zina mifumo ya kuongeza joto nyumbani ambayo inazifanya ziwe na joto ndani hata wakati wa majira ya baridi. Nyumba lazima ziwe safi, ziwe na madirisha yote na zisiwe na wadudu/wanyama waharibifu. Nyumba ina vifaa vya kupika, kula, kulala na kuoga.

Vitu ambavyo hupatikana nyumbani kwa kawaida

 • vitanda na magodoro
 • mablangeti na pilo
 • meza na viti vya jikoni
 • friji na jiko
 • vifaa vya bafuni kama vile choo, sehemu ya kuoshea mikono na bafu la manyunyu
 • vifaa vya kupika vyakula rahisi, kama vile sufuria, pani, sahani na vyombo vya kutumia kula mezani.

Vifaa ambavyo havichukuliwi kuwa vya msingi ni televisheni na kompyuta. Unaweza kununua viti na meza zaidi na vitu vingine unavyohitaji baadaye, lakini mara nyingi unahitaji kuweka akiba ya kuvinunua.

Jikoni iliyo na mfumo wa sinki, sinki, kabati na friji

Picha: Manispaa ya Nordanstig

Choo kilicho na kiti, beseni ya kuoshea mikono na kioo.

Picha: Manispaa ya Nordanstig

Eneo la makazi lenye nyumba za kukodisha.

Picha: Shirika la Uhamiaji la Uswidi (Migrationsverket, The Swedish Migration Agency)/Björn Bjarnesjö

Kukodisha nyumba

Unalipa kodi ya nyumba yako kila mwezi. Unaweza kuomba msaada wa fedha wa kukusaidia kulipa kodi yako ya nyumba. Kiasi cha kodi ya nyumba kinatofautiana kati ya nyumba tofauti, lakini sehemu kubwa ya msaada wako wa fedha itatumika kulipa kodi ya nyumba. Gharama ya kodi ya nyumba itaelezwa kwenye mkataba wako wa kukodisha nyumba. Mkataba wa kukodisha nyumba ni hati unayotia saini unapohamia kwenye nyumba yako. Mkataba wa kukodisha nyumba unaeleza pia maelezo mengine, kama vile muda wa kuishi kwenye nyumba na siku ya mwisho ya kulipa kodi yako ya nyumba.

Kampuni za nyumba za kukodisha kwa kawaida huwa na orodha ya wanaotafuta nyumba, ambayo ni orodha ya wanaotafuta nyumba za kukodisha zinazopatikana. Ni kawaida kusubiri kwenye foleni kwa muda mrefu kabla ya kupata nyumba ya kukodisha. Kwa hivyo ni vyema ikiwa utajiandikisha kwenye kampuni ya nyumba za kukodisha haraka iwezekanavyo. Unaweza kuomba mwakilishi wa manispaa yako akupe maelezo zaidi kuhusu jinsi ya kujiunga kwenye orodha ya wanaosubiri nyumba za kukodisha.

Kanuni za kawaida

Katika majengo mengi ya nyumba za kukodisha kuna kanuni za kawaida ambazo kila mtu lazima afuate.

 • Kuna kanuni za kuzuia mioto. Unapikia chakula chako kwenye stovu na jiko la umeme. Usiwahi kuacha stovu au jiko lako la umeme bila kuangaliwa. Ikiwa unataka kuchoma nyama au kuwasha moto, fanyia katika sehemu maalum nje ya nyumba na kwa uangalifu mkubwa. Unaweza kuwasha mishumaa ndani ya nyumba lakini lazima uizime kabla ya kuondoka nyumbani au kwenda kulala. Watoto hawapaswi kabisa kucheza na moto, viberiti au vifaa vya kuwasha sigara.
 • Kampuni nyingi za nyumba za kukodisha zina sera ya kutoruhusu uvutaji sigara katika nyumba zake, iwe katika nyumba ya mtu binafsi au katika maeneo ya umma.
 • Majengo mengi ya nyumba za kukodisha yana kanuni kuhusu kelele za juu, hasa jioni na usiku. Hakupaswi kuwa na kelele wakati fulani jioni na wakati wa usiku.
 • Makazi yote yana maeneo yaliyotengwa ambapo wakazi wanaweza kutupa taka. Huruhusiwi kuacha taka au mifuko ya taka mbele ya maeneo ya umma au nje ya nyumba. Nchini Uswidi, ni kawaida kuchuja taka ya nyumbani, yaani kuchuja na kutenganisha taka yako.
 • Majengo mengi ya nyumba za kukodisha yana vyumba vya kufulia nguo pamoja vilivyo na mashine za kufua ambazo wakazi wa jengo hilo wanaweza kutumia. Kwa kawaida unahitaji kuhifadhi wakati mapema ikiwa unataka kutumia chumba cha kufua nguo. Chumba cha kufua nguo hutunzwa na kila mtu anayeishi katika jengo hilo na lazima kiachwe kikiwa safi baada ya kumaliza shughuli ya kufua nguo.
 • Una jukumu la kumjulisha mwenye nyumba ikiwa kitu chochote cha nyumbani kimevunjika au kimeharibika. Kwa mfano, ikiwa sakafu, friji au mlango utavunjika. Ikiwa unahama katika nyumba yako, lazima iwe katika hali uliyoipata ulipohamia humo, vinginevyo unaweza kulazimika kulipa gharama za ukarabati.
 • Una jukumu la kumjulisha mwenye nyumba ikiwa utagundua kuna wadudu/wanyama waharibifu nyumbani.
 • Unawajibika kwa nyumba yako unapohamia humo. Usipotii kanuni zilizo kwenye mkataba au usipolipa kodi ya nyumba kwa wakati unaofaa, inaweza kusababisha upoteze nyumba yako.
Ishara inayoonyesha kwamba huruhusiwi kuvuta sigara.

Ishara inayoonyesha kwamba huruhusiwi kuvuta sigara. Picha: Shirika la Uhamiaji la Uswidi (Migrationsverket, The Swedish Migration Agency)/Björn Bjarnesjö

Last updated: