Haki na wajibu wa watu wote nchini Uswidi

Rättigheter och skyldigheter för alla i Sverige – swahili

Kwenye ukurasa huu unaweza kusoma maelezo kuhusu haki zako kama mwananchi wa Uswidi, na pia wajibu wako kwa wengine.

Muhtasari

  • Uswidi ni nchi ya kidemokrasia yenye ufisadi mdogo ambapo watu wote ni sawa mbele ya sheria.
  • Uswidi ni taifa lisilohusishwa na dini yoyote, kumaanisha kwamba sheria na maamuzi ya kisiasa yametofautishwa na dini.
  • Nchini Uswidi, watu wote ni sawa na wana haki sawa bila kujali jinsia, umri, mwelekeo wa kuvutiwa kimapenzi, msingi wa kikabila, dini au ulemavu. Kila mtu ana haki juu ya maisha na mwili wake, bila kuingiliwa na jamii au watu wengine, ikiwa ni pamoja na familia zao.
  • Ni muhimu haki hizi ziheshimiwe. Nchini Uswidi, kuwadhulumu wanawake au kumbagua mtu fulani kwa msingi wa mwelekeo wa kuvutiwa kimapenzi ni kosa.
  • Nchini Uswidi, kila mtu mwenye umri wa chini ya miaka 18 ni mtoto kisheria. Kuna sheria kadhaa zilizopo za kuwalinda watoto na kuwahakikishia malezi salama yasiyo ya kudhulimiwa, ajira ya watoto na ndoa za kulazimishwa. Unaweza kuadhibiwa kwa kukiuka haki za watoto au, kwa mfano, mtoto anaweza kupelekwa katika kituo cha matunzo.
  • Ikiwa unahisi kwamba ni vigumu kuwa mzazi mlezi, unaweza kupata usaidizi na msaada kutoka kwa jamii, kwa mfano, kituo cha afya, shuleni na katika shirika la huduma ya ustawi wa jamii. Huduma ya ustawi wa jamii nchini Uswidi ipo ili kuwasaidia wazazi walezi na watoto ili familia iweze kuishi pamoja kwa furaha.

Ni kupitia kwa sheria ambapo unahakikishiwa uhuru na haki fulani nchini Uswidi, lakini pia kuna wajibu ambao wewe, kama mwananchi wa Uswidi lazima uuwajibikie na kuufuata. Lazima pia uheshimu haki za wengine na unatarajiwa kuchangia katika jamii.

Kutii sheria

Wewe kama mwananchi wa Uswidi, bila kujali utaifa, utamaduni, hadhi katika jamii au dini, lazima ufuate sheria za Uswidi.

Nchini Uswidi, mtu yeyote anayeshukiwa kufanya kosa anachukuliwa kuwa hana hatia hadi apatikane na hatia.

Watu wanaovunja sheria wanaweza kushtakiwa na kufungwa jela kulingana na sheria zinazohusika. Hukumu ya makosa ya uhalifu inaweza kuwa kupigwa faini, kulipa fidia au kufungwa jela.

Haiwezekani kutoa hongo ili kuhepa au kupewa hukumu ndogo. Kumhonga afisa ni kosa nchini Uswidi. Kuna kiwango cha chini cha ufisadi nchini Uswidi, ambayo pia inamaanisha kwamba huwezi kutoa hongo ili kupata kazi, gredi au cheti haraka na huduma bora ya afya.

Kuheshimu haki za binadamu

Jamii ya Uswidi inatilia maanani sana uhuru na usawa wa kibinafsi. Kwa hivyo kila mtu nchini Uswidi ana haki sawa na lazima atendewe kwa usawa, bila kujali jinsia, kabila, maoni ya kidini, mwelekeo wa kingono au ulemavu wa kimwili. Hakuna mtu anayepaswa kufanyiwa ukatili, kutendewa vibaya, kutishiwa au kulazimishwa kuishi maisha ambayo hataki.

Uhuru wa dini

Kila mtu nchini Uswidi ana haki ya kuchagua na kufuata dini au imani anayotaka. Kila mtu ana haki ya kutoamini dini yoyote, kubadili dini yake au kuiacha. Kuwa na uwezo wa kuchagua dini au imani unayotaka ni haki ya binadamu. Kuna sheria zinazolinda haki ya kuwa na dini au imani yoyote unayotaka.

Usawa wa kijinsia

Usawa unahusu wanawake, wanaume na watu wa jinsia tofauti kuwa na haki, fursa na wajibu sawa. Kila mtu, bila kujali jinsia, ana haki sawa ya kuenda shule na anahitaji kuwajibika kwa njia sawa kwa nyumba na watoto.

Haki za walio wachache kijinsia

Nchini Uswidi, kila mtu ana haki ya kupenda, kukutana, kuishi na au kuoa yeyote anayetaka. Una haki ya kuoa mtu wa jinsia sawa au wa jinsia tofauti. Kuna sheria zinazolinda haki yako ya kumpenda unayemtaka na ni kinyume cha sheria kumbagua mtu yeyote kulingana na mwelekeo wake wa kingono.

Bendera ya Pride na wanaume wawili wakibusiana.

Tamasha la Pride ni tukio kubwa nchini Uswidi ambalo husherehekea haki ya kila mtu kumpenda anayetaka na kuwa jinsi alivyo. Picha: Sofia Sabel/imagebank.sweden.se

Ukatili wa kijinsia

Hakuna mtu anayepaswa kulazimishwa kuwa jinsi ambavyo hataki kuwa. Hakuna mtu anayeweza kulazimishwa katika kanuni, wajibu au vizuizi fulani vya kijinsia kwa sababu ya mwelekeo wa kijinsia au kingono. Kulazimisha mtu kuishi kwa njia fulani au kumzuia mtu kwa sababu ya mwelekeo wa kijinsia au kingono ni uhalifu nchini Uswidi.

Uswidi imepiga hatua kubwa katika jitihada zake za usawa wa kijinsia, lakini bado kuna kazi nyingi za kufanya. Ukatili wa kijinsia huathiri wanawake kwa kiwango kikubwa kuliko wanaume. Unaweza kuwa wa kimwili, kisaikolojia, kihisia, maneno, kijamii au kifedha. Kwa mfano, kutishia au kumzuia mtu kuwasiliana na watu wengine, au kumlazimisha mtu kufanya ngono bila kupenda.

Ndoa ya kulazimishwa

Nchini Uswidi, ni kosa la jinai kumlazimisha mtu kuoa kinyume na mapenzi yake. Kujaribu na kujiandaa kwa ndoa ya kulazimishwa pia ni hatia, sawa na kumdanganya mtu kusafiri nje ya nchi kwa madhumuni ya kumwoza kwa nguvu au kumtumia vibaya.

Ukeketaji wa wanawake (FGM)

Ukeketaji wa wanawake unachukuliwa kuwa ukatili wa kijinsia. Kutekeleza ukeketaji wa wanawake ni uhalifu mkubwa nchini Uswidi na pia kumshawishi mtu mwingine aitekeleze. Ni hatia kuficha taarifa kuhusu ukeketaji wa wanawake uliopangwa. Ikiwa una taarifa kwamba ukeketaji wa wanawake umepangwa kufanywa, unapaswa kujulisha mamlaka za Uswidi.

Iwapo wewe au mtu unayemjua amenyanyaswa, lazima uripoti kwa polisi kwa kupiga simu 114 14. Piga 112 ikiwa ni jambo la dharura. Unaweza pia kuwasiliana na kituo cha polisi mahali ulipo.

Msaada unapatikana ikiwa wewe ni mwathiriwa wa unyanyasaji:

  • Manispaa yako ina jukumu la kulinda watu wanaokabiliwa na vurugu kwa kuwapa makazi.
  • Huduma ya ustawi wa jamii ipo kwa ajili ya kutoa usaidizi na kuwasaidia watoto na watu wazima wanaoishi na ukatili katika mahusiano ya karibu na unyanyasaji na ukandamizaji unaohusiana na heshima.
  • Nchini Uswidi kuna makazi ya wanawake yanayotoa usaidizi na ulinzi kwa wanawake na watoto ambao wamenyanyaswa katika mahusiano ya karibu au unyanyasaji na ukandamizaji unaohusiana na heshima. Makazi ya wasichana yanapatikana kwa vijana.
  • Katika manispaa nyingi kuna vituo vya migogoro vinavyowasaidia watu ambao wamenyanyaswa au kuwasaidia wanaume kuacha vurugu. Ukikabiliwa na vitisho na vurugu, unaweza kupiga simu kwa Kvinnofridslinjen (nambari ya usaidizi ya kitaifa kwa wanawake wa Uswidi) iliyo wazi kila wakati. Ni bure kupiga simu na huhitajiki kusema jina lako unapopiga. Nambari ya simu ni 020-50 50 50.

Soma zaidi kwenye tovuti ya Kvinnofridslinjen (kwa Kiingereza) External link, opens in new window.

Soma zaidi kwenye tovuti ya Polisi (kwa Kiingereza) External link, opens in new window.

Haki za watoto

Kulingana na sheria ya Uswidi, watu wote walio chini ya umri wa miaka 18 wanazingatiwa kuwa watoto. Watoto nchini Uswidi wana haki ya elimu, afya, usalama na malezi bora. Watoto wana haki ya kueleza mawazo yao, hisia na wasiwasi. Maoni yao ni muhimu katika masuala yanayowahusu, ingawa wazazi wanaomlea mtoto wana jukumu la kuamua ni nini kinachomfaa mtoto.

Nchini Uswidi, ni marufuku kupiga au kuwaadhibu watoto kimwili. Unaweza kusoma kuhusu jambo hilo na mengi zaidi katika Mkataba wa Haki za Mtoto (Barnkonventionen, Convention on the Rights of the Child) (CRC), ambayo ni sheria ya Uswidi.

Soma kuhusu haki za watoto kwenye tovuti ya Ombudsman for Children (Kwa Kiswidi) External link, opens in new window.

Soma kuhusu Mkataba wa Haki za Mtoto (Barnkonventionen, Convention on the Rights of the Child) (Kwa Kiingereza). External link, opens in new window.

Bango kuhusu Mkataba wa Haki za Mtoto (Barnkonventionen, Convention on the Rights of the Child) (Kwa Kiingereza) External link, opens in new window.

Shirika la Uhamiaji la Uswidi (Migrationsverket, The Swedish Migration Agency) pia hutoa taarifa inayowalenga watoto. Tafadhali jisikie huru kusoma peke yako au pamoja na mtoto wako kuhusu jinsi maisha ilivyo kwa watoto nchini Uswidi.

Jukumu la huduma ya ustawi wa jamii

Ikiwa uhusiano kati yako na mtoto wako ni mbaya au una wasiwasi kuhusu tabia ya mtoto wako, unaweza kuwasiliana na huduma ya ustawi wa jamii katika manispaa yako, shule ya chekechea au ya msingi ya mtoto wako au mfumo wa huduma ya afya.

Huduma ya ustawi wa jamii hufanya kazi pamoja na famila ili kusaidia familia na ustawi wao. Wakati mwingine huduma ya ustawi wa jamii huhitajika kuingilia kati na kuwatunza watoto walio hatarini, lakini huduma ya ustawi wa jamii haitawajali watoto wako mara moja ikiwa familia yako ina matatizo au inahitaji usaidizi.

Kutenganisha mtoto kutoka kwa wazazi wake hufanywa katika hali za kipekee kwani inaweza kuwa uzoefu mgumu sana kwa mtoto. Inatokea wakati ni hatari zaidi kwa mtoto kubaki na wazazi wake kuliko kutengwa nao, kwa mfano, ikiwa mtoto anatelekezwa au kunyanyaswa vibaya.

Huduma ya ustawi wa jamii hupatikana katika kila manispaa. Wanafanya kazi chini ya sheria inayoitwa Sheria ya Huduma za Jamii. Sheria ya Huduma za Jamii inahusu haki ya huduma ya afya ambayo kila mtu katika manispaa anayo. Ina sheria kuhusu jinsi jamii inapaswa kuwasaidia wanaohitaji msaada, lakini hawawezi kupata msaada kutoka kwa mtu mwingine yeyote.

Soma zaidi kuhusu dhamira ya huduma ya ustawi wa jamii:

Maswali na majibu ya malezi ya watoto kwa mujibu wa sheria na masharti maalum kuhusu malezi ya vijana (Kwa Kiswidi) External link, opens in new window.

Ndoa za utotoni

Ndoa ambapo mtu mmoja au wote wawili wako chini ya umri wa miaka 18 ni uhalifu nchini Uswidi na ni batili kisheria, hata ikiwa imekuwa halali katika nchi ambayo ndoa ilifanyika. Mwingiliano wowote wa kingono na watoto walio chini ya umri wa miaka 15 ni uhalifu na mtu anayetekeleza kitendo hicho anaweza kuhukumiwa kwa kosa la ngono. Hata baada ya umri wa miaka 15, kila mtu ana haki ya kujichagulia iwapo anataka kushiriki katika shughuli za kingono na nani. Hii pia inatumika kwa watu ambao wako katika uhusiano, wameoana au wanaishi pamoja.

Maswali ya kuzingatia

  • Tunatakiwa kuheshimu sheria na maadili ya nchi tulipo. Je, unahisi kwamba unahitaji taarifa zaidi kuhusu jinsi inavyofanya kazi nchini Uswidi ili kuelewa vyema?

Last updated: