Safari yako ya kuelekea nchini Uswidi

Din resa till Sverige – swahili

Kwenye ukurasa huu unaweza kupata maelezo kuhusu kinachotendeka kabla, wakati na baada ya safari yako ya kuelekea nchini Uswidi.

Muhtasari

 • Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM, International Organization for Migration) na Shirika la Uhamiaji la Uswidi (Migrationsverket, The Swedish Migration Agency) yatapanga safari yako ya kuelekea nchini Uswidi. Shirika la IOM litakujulisha tarehe yako ya kusafiri na kukupa maelezo mengine muhimu. Utapokea hati zote muhimu za kusafiri kabla ya kuondoka.
 • Huwezi na kuja na mali yote nchini Uswidi. Pakia tu vitu muhimu unavyohitaji. Shirika la IOM litakujulisha kuhusu idadi ya begi unazoruhusiwa kubeba na uzito wake.
 • Unapaswa kupakia kila kitu unachohitaji katika safari yako kwenye begi yako ya mkononi.
 • Mwakilishi kutoka katika manispaa yako atakukaribisha katika uwanja wa ndege au unapowasili katika manispaa yako. Wakati mwingine, manispaa yako itakutumia teksi katika uwanja wa ndege itakayokupeleka katika makao yako.
 • Utapewa begi ya IOM itakayomsaidia mwakilishi kutoka katika manispaa yako nchini Uswidi na mfanyakazi wa uwanja ndege kukutambua katika uwanja wa ndege. Beba begi ya IOM na uhakikishe inaonekana katika safari nzima.

Utasafiri kwa ndege kwenda nchini Uswidi. Shirika la IOM na Shirika la Uhamiaji la Uswidi (Migrationsverket, The Swedish Migration Agency) yatapanga safari yako, kukujulisha tarehe yako ya kusafiri na kukupatia hati zako za kusafiri. Ni jukumu lako kufika katika uwanja wa ndege wa safari yako. Wakati mwingine unaweza kusaidiwa kufika huko na shirika la IOM.

Jiandae kwa safari ndefu. Huenda utahitaji kubadilisha ndege. Safari ya ndege pia inahusisha vipindi vya kungoja na kupanga foleni katika viwanja vya ndege.

Ukifika katika uwanja wa ndege wa mahali unakoenda nchini Uswidi, kwa kawaida utasafiri kwa gari, wakati mwingine kwa basi hadi katika makao yako. Jumla ya muda wa kusafiri kutoka katika nchi ambayo unatoka hadi katika makao yako mapya nchini Uswidi inaweza kuchukua zaidi ya siku moja. Jaribu kupumzika na kupata usingizi wa kutosha kabla ya kuanza safari.

Mwonekano kutoka kwenye ndege.

Mwonekano kutoka kwenye ndege. Picha: Shirika la Uhamiaji la Uswidi (Migrationsverket, The Swedish Migration Agency)

Kupakia mizigo yako ya safari ya kuelekea Uswidi

Idadi ya begi na uzito wake

Kuna kikomo cha idadi ya begi za kubeba kwenye ndege na uzito wa begi hizo. Vikomo hivi huwekwa na kampuni ya shirika la ndege unayosafiri nayo. Mashirika tofauti ya ndege yana vikomo tofauti, lakini ni kawaida kwa kila msafiri kubeba begi moja kubwa na begi moja ndogo (kwa mfano, begi ya nguo na begi ya mgongoni). Shirika la IOM litakujulisha idadi ya begi unazoweza kubeba na uzito wake.

Vitu vya kupakia

Ni muhimu ufikirie kuhusu vitu unavyohitaji zaidi kwenda navyo nchini Uswidi, kwa sababu idadi ya begi unazoruhusiwa kubeba kwenye ndege ni chache.

Vyombo vya jikoni na vitu vingine vya mbao viko katika nyumba yako mpya, kwa hivyo huhitaji kubeba vitu kama hivyo. Hata hivyo, ni hakika kwamba utataka kubeba picha za familia na vitu vingine vya binafsi ambavyo ni muhimu kwako.

Kuna pia kanuni kuhusu vitu unavyoweza kuweka katika mzigo wako na kusafiri navyo kuelekea Uswidi. Shirika la IOM litakujulisha kuhusu vitu ambavyo huruhusiwi kubeba. Kuna kifaa cha kuchunguza katika uwanja wa ndege ambacho hupekua mzigo ili kupata vitu ambavyo haviruhusiwi.

Mizigo iliyokaguliwa

Begi yako kubwa hukaguliwa katika uwanja wa ndege na itawekwa katika sehemu ya kubeba mizigo ya ndege katika safari nzima. Utapeana begi yako kwa mfanyakazi katika uwanja wa ndege unakoabiria ndege, na kwa kawaida hutapewa hadi ufike nchini Uswidi. Mfanyakazi wa uwanja wa ndege ataweka kibandiko kwenye begi yako kinachoonyesha kwamba ni yako, mahali ambapo unaelekea na ndege utakayoabiri ili begi yako iwekwe kwenye ndege sahihi.

Unapaswa kupakia vitu ambavyo huhitaji katika safari yako kwenye begi yako kubwa ya kukaguliwa, kama vile nguo.

Begi ya mkononi

Unaweza kuwa na begi yako ndogo ya mkononi katika safari nzima. Kwenye begi ya mkononi, unaweka kila kitu unachoweza kuhitaji katika safari.

Hivi ndivyo vitu unavyohitaji kupakia kwenye begi yako ya mkononi:

 • Hati zako za kusafiri, tiketi, pesa, pasipoti na hati zingine za kitambulisho, kwa sababu utavihitaji katika safari.
 • Hati zingine muhimu, kama vile vyeti, dawa na rekodi za matibabu.
 • Dawa unazohitaji na unazoruhusiwa kubeba kwenye ndege. Ikiwa umeandikiwa dawa na daktari, ni vyema ubebe dawa ya kutosha kwa siku 30 kwa sababu hutaweza kupata dawa au dawa mpya za kuandikiwa na daktari moja kwa moja nchini Uswidi.
 • Vitu vya kuwafurahisha watoto kwenye ndege, kama vile vitu vya kuchezea.
 • Chakula cha mtoto, maziwa ya mtoto, uji au vyakula vyepesi ikiwa unasafiri na watoto wachanga au watoto wadogo.

Unapaswa kuvaa nguo ambazo zinafaa kwa msimu uliopo nchini Uswidi, au uzipakie kwenye begi yako ya mkononi.

Soma maelezo kuhusu misimu ya nchini Uswidi, hali ya hewa na mavazi ya msimu

Hata ukisafiri kuelekea nchini Uswidi wakati kuna joto, ni vyema upakie sweta kwenye begi yako ya mkononi ili uwe salama tu kwa sababu kunaweza kuwa na baridi ndani ya ndege.

Begi ya IOM

Utapewa begi ya IOM kabla ya kuanza safari. Ina maelezo na hati muhimu. Beba begi ya IOM mkononi na uhakikishe inaonekana kila wakati. Kuna wafanyakazi watakaokuelekeza katika viwanja vya ndege, unapobadilisha ndege na unapofika nchini Uswidi. Begi ya IOM inapoonekana inafanya iwe rahisi kwa wafanyakazi kukutambua.

Picha inayoonyesha mwonekano wa begi ya IOM.

Begi ya IOM. Picha: IOM/Alex Van Hagen

Wakimbizi wanaohamia nchi nyingine katika uwanja wa ndege kabla ya kuanza safari yao.

Wakimbizi wanaohamia nchi nyingine katika uwanja wa ndege wakingoja kuondoka. Picha: IOM/Rami Ibrahim

Hatua mbalimbali katika safari yako ya kuelekea Uswidi

Katika uwanja wa ndege

Unapita katika vituo kadhaa vya ukaguzi katika uwanja wa ndege kabla ya kuruhusiwa kuabiri ndege. Kwa hivyo, ni muhimu ufike katika uwanja wa ndege mapema kabla ya ndege kuondoka. Shirika la IOM litakujulisha wakati unaopaswa kuwa katika uwanja wa ndege na wakati mwingine wanaweza kuambatana nawe kwenda huko au kukujulisha jinsi ya kufika huko mwenyewe.

Kabla hujaabiri ndege, unapaswa kuripoti kwenye kituo sahihi cha huduma. Katika kituo cha huduma, utapewa cheti cha abiria kinachoeleza lango ambalo ndege unayoabiri inaondokea, wakati wa kuanza kuabiri ndege na kiti chako kwenye ndege. Utapeana pia mzigo wako, ambapo utakaguliwa kisha kupakiwa kwenye ndege.

Utapitia katika kituo cha ukaguzi wa usalama ambapo wewe na begi yako ya mkononi itakaguliwa ili kuona ikiwa umebeba vitu vyovyote hatari au visivyoruhusiwa. Kuna pia ulinzi wa mipakani ambapo hati zako zitakaguliwa.

Baada ya kupita katika ukaguzi huu wote, utahitaji kutafuta kituo chako cha kuabiri ndege, ambacho ni sehemu ya uwanja wa ndege ambapo ndege unayoabiri itaondokea. Kuna skrini na ishara katika uwanja wa ndege za kukusaidia utambue kituo sahihi cha kuabiria ndege na lango sahihi ndani ya kituo.

Ukibadilisha ndege katika safari yako ya kuelekea Uswidi, ukaguzi fulani hufanywa tena katika uwanja wa ndege ambapo unabadilisha ndege. Mara nyingi kuna mtu ambaye anaweza kukuelekeza unaposhuka kwenye ndege. Ni muhimu uhakikishe begi ya IOM inaonekana ili mtu huyo aweze kukutambua.

Ukiwa katika safari ya ndege

Kila abiria kwenye ndege atakuwa na kiti chake. Unaweza kuona nambari ya kiti chako kwenye cheti chako cha abiria. Unaweza kuomba mfanyakazi kwenye ndege akusaidie kupata kiti chako. Baada ya kupata kiti chako, unaketi, kujifunga mkanda wa usalama na kungoja kuanza safari.

Kwenye ndege, watoto huketi pamoja na watu wazima wanaosafiri nao. Watoto wenye umri wa chini ya miaka miwili huketi kwenye miguu ya mtu mzima anayesafiri naye. Wakati wa safari ya ndege, mtu mzima ana jukumu la kuhakikisha mtoto ameketi ipasavyo kwenye kiti chake. Kukimbiakimbia hakuruhusiwi kwenye ndege, na hakuna sehemu ya watoto kwenye ndege.

Kabla ya ndege kupaa, wahudumu wa safari ya ndege hutoa maagizo kuhusu cha kufanya wakati wa dharura.

Wakati wa safari yako ya ndege, lazima ubaki umeketi kwenye kiti chako kadri iwezekanavyo. Kuna vyoo vya kutumia kwenye ndege. Vyakula na vinywaji huandaliwa katika safari ndefu za ndege. Inaweza kuwa vyema kulala katika safari ndefu za ndege kwa sababu safari ya kuelekea katika makao yako mapya ni ndefu.

Kufika nchini Uswidi

Unapofika nchini Uswidi, unahitaji kupitia katika kituo cha ulinzi wa mpakani na uchukue mzigo wako uliokaguliwa. Mfanyakazi katika uwanja wa ndege atakukaribisha na kukuelekeza. Atakuambia mahali pa kwenda baada ya kushuka kwenye ndege. Kumbuka kuhakikisha begi ya IOM inaonekana.

Wakati mwingine unaweza kubadilisha ndege hata ukiwa nchini Uswidi ili ufike mahali unapoenda. Kutoka kwenye uwanja wa ndege, kwa kawaida unasafiri kwa gari. Uswidi ni nchi kubwa kwa hivyo unaweza kuhitaji kusafiri kwa muda mrefu baada ya kushuka ili ufike katika manispaa yako.

Mwakilishi kutoka katika manispaa yako atakukaribisha katika uwanja wa ndege au unapowasili katika manispaa yako. Wakati mwingine, manispaa yako itakutumia teksi katika uwanja wa ndege itakayokupeleka katika makao yako. Unapofika katika manispaa ya makao yako, utaonyeshwa makao yako na kuelezwa kitakachofanyika baadaye.

Mkanda wa mizigo katika sehemu ya kuchukua mizigo.

Sehemu ya kuchukua mizigo. Picha: Mostphotos

Maswali ya kuzingatia

 • Umekuwa ukifikiria kuhusu vitu utakavyozingatia kupakia?
 • Je, unajua tofauti kati ya mzigo wa kukaguliwa na kuwekwa na mzigo wa kubeba mkononi?

Last updated: