Maisha ya kila siku

Vardagsliv – swahili

Kwenye ukurasa huu unaweza kusoma maelezo kuhusu jinsi maisha ya kila siku nchini Uswidi yanavyoweza kuwa, kwa mfano unachoweza kununua, maoni kuhusu kutumia tena vitu na shughuli za mapumziko.

Muhtasari

  • Kujifunza Kiswidi kutakusaidia kufaulu katika elimu yako, kupata kazi na kuwa na marafiki. Kuna kozi za lugha katika viwango tofauti.
  • Huduma nyingi nchini Uswidi ni za mtandaoni. Ni faida kwako ikiwa utajifunza kutumia simu mahiri au kompyuta.
  • Ni muhimu utunze afya yako ya mwili na akili. Ikiwa hali yako ya afya inahitaji matibabu, unaweza kuweka miadi na umwone daktari.
  • Ni vyema kutenga baadhi ya muda wako wa ziada kufanya shughuli tofauti na mambo unayopenda. Ni njia ya kutangamana kwa urahisi na watu wengine na kujifunza lugha ya Kiswidi.
  • Ni rahisi, salama na nafuu kutumia usafiri wa umma nchini Uswidi. Watu wengi husafiri kwenda na kutoka kazini au shuleni kwa basi au treni.
  • Lazima uwe na umri wa miaka 18 na uwe na leseni ya udereva iliyoidhinishwa ili uendeshe gari nchini Uswidi. Ni lazima kila mtu afunge mikanda ya usalama na mikanda ya usalama ya watoto, inayotumika unapoendesha gari ukiwa na watoto wadogo.
  • Nchini Uswidi, ununuzi mwingi wa chakula, nguo na vitu vya samani (viti, meza, vitanda) hufanywa katika maduka makubwa au madogo ukiwa nyumbani au katika maduka mbalimbali ambayo kwa kawaida yanapatikana katika miji mikubwa.
  • Mabaki ya vitu kutoka kwenye taka hutumiwa kutengeneza bidhaa mpya na ni sehemu muhimu ya kazi ya utunzaji mazingira nchini. Lazima uchuje mwenyewe vitu kama vile taka ya chakula, plastiki, chuma na glasi.

Umuhimu wa kuji­funza Kiswidi

Kwa vile unahamia nchini Uswidi inamaanisha kwamba unahitaji kujifunza Kiswidi. Kiswidi ni lugha rasmi na huzungumzwa kila mahali. Itakuwezesha kutangamana na wengine nchini ikiwa utaanza kujifunza Kiswidi mara moja baada ya kufika nchini Uswidi. Kuelewa na kuzungumza Kiswidi kunakusaidia kutafuta kazi, kuanza masomo, kupata huduma za umma na kujuana na watu. Kama mgeni nchini Uswidi, utajifunza Kiswidi kama sehemu ya mpango wa msaada wa makaribisho. Kuna pia zana nyingi dijitali na vituo vya lugha vinavyokusaidia kujifunza Kiswidi.

Hapa unaweza kuona fursa tofauti zinazopatikana za kujifunza Kiswidi (kwa Kiingereza) External link, opens in new window.

Jamii dijitali

Uswidi ni nchi inayoendelea kuwa dijitali zaidi. Teknolojia inatumika kila mahali katika jamii, shuleni, kazini na wakati wa mapumziko. Kazi nyingi zinahitaji ujuzi wa msingi wa kompyuta. Katika familia nyingi nchini Uswidi, watoto wanamiliki simu mahiri au kompyuta za binafsi (laptop). Watu wazima hutumia simu mahiri kulipa bili zao, kupata huduma za benki, kuweka miadi mbalimbali, kununua tiketi na kwa utambulisho wa kielektroniki. Kujifunza kutumia huduma dijitali ni muhimu ili kuzoea maisha ya kila siku nchini Uswidi.

Intaneti pia hutumika kutafuta habari. Ni muhimu utumie vyanzo vya kutegemewa, kama vile tovuti rasmi za serikali, kwa sababu kuna habari nyingi za uongo na za kupotosha na uvumi unaoenezwa katika mitandao jamii na kwenye intaneti. Ikiwa huna kompyuta yako binafsi au muunganisho wa intaneti, unaweza kutembelea maktaba na utumie kompyuta bila malipo. Katika maeneo mengine ya umma, unaweza pia kutumia intaneti ya bure kwa kuunganisha simu yako mahiri au kompyuta ya binafsi (bärbara dator, laptop).

Ikiwa unahitaji usaidizi wa jinsi ya kutumia vifaa dijitali au huduma mbalimbali dijitali, maktaba, mashirika ya kujitolea au manispaa kwa kawaida hutoa usaidizi au kozi za msingi.

Kvinna med mobiltelefon.

Kutunza afya yako

Kuhamia katika nchi mpya kuna mabadiliko na changamoto nyingi na inaweza kuhitaji ubadilishe mtindo wako wa maisha. Ili kuhakikisha kwamba unaendelea kuwa mzima, ni muhimu utunze afya yako ya mwili na akili. Kuna vitu unavyoweza kufanya mwenyewe ili kutunza afya yako, kama vile kupata usingizi wa kutosha, kula vyakula bora na kufanya mazoezi.

Ikiwa una ugonjwa unaohitaji matibabu, unaweza kuweka miadi na umwone daktari. Daktari anaweza kukuandikia dawa au matibabu mengine yanayowezesha au kuboresha hali yako.

Shughuli za mapumziko

Shughuli za mapumziko zinakupa fursa ya kufanya mambo unayopenda, kukutana na watu, kujumuika na jamii na fursa ya kujifunza lugha ya Kiswidi.

Shughuli nyingi za mapumziko zinaweza kufanywa bila kujali umri na jinsia. Kuna shughuli ambazo zinalenga zaidi rika au jinsia fulani, kwa mfano mizunguko tofauti ya mafunzo ya watu wazima au kuogelea kwa wanawake. Kuna shughuli za mapumziko za watoto za rika mbalimbali.

Aina ya shughuli za mapumziko katika manispaa mbalimbali ni tofauti. Shughuli nyingine hazilipishwi ilhali nyingine zinalipishwa. Maeneo mengi ya umma ni bure kuingia. Haya yanaweza kuwa, k.m, viwanja vya michezo, majengo ya mazoezi ya mwili ya nje, maeneo ya michezo ya kuteleza pamoja na mabustani na maeneo ya kupendeza ya umma.

Kujisa­fi­risha

Kutumia usafiri wa umma, k.m, kwa basi, treni au treni ya chini kwa chini, ni njia ya kawaida ya kusafiri nchini Uswidi na watu wengine huitumia kila siku kwenda kazini au shuleni. Usafiri wa umma ni salama, rahisi kutumia na nafuu kuliko kutumia gari lako binafsi. Miji yote inaweza kufikiwa kwa basi au treni, na katika miji mikubwa kiasi kuna treni, tramu au treni ya chini kwa chini.

Unaweza kununua tiketi za usafiri wa umma kabla ya kuabiri. Unaweza kuzinunua katika maduka madogo mbalimbali au mashine za tiketi zinazohusiana na usafiri wa umma. Mara nyingi unaweza kununua tiketi kupitia programu kwenye simu yako mahiri. Ukisafiri bila tiketi, unaweza kupigwa faini.

Kusa­firi kwa bais­keli

Wakati safari si ya mbali sana, baiskeli ndio hutumiwa zaidi nchini Uswidi. Katika miji kuna barabara maalum za baiskeli.

Unahitaji kujua sheria za barabarani zinazotumika, k.m, kwamba magari ni ya mkono wa kulia. Kisheria, baiskeli lazima iwe na taa na riflekta kukiwa na giza. Kwa sababu za usalama, watoto wenye umri wa chini ya miaka 15 lazima wavae helmeti, lakini ni faida ikiwa kila mtu anayeendesha baiskeli atavaa helmeti kwa sababu mara nyingi unapita kwenye barabara yenye shughuli nyingi.

Ni muhimu kutumia riflekta ili uweze kuonekana kukiwa na giza na uwe makini wakati barabara zina barafu na zinateleza.

Kuen­desha gari

Ikiwa unataka kuendesha gari nchini Uswidi, lazima uwe na angalau umri wa miaka 18 na uwe na leseni ya udereva ambayo imeidhinishwa nchini Uswidi. Mtu yeyote anayesafiri kwenye gari lazima afunge mkanda wa usalama, na watoto wasiozidi urefu wa sentimita 135 lazima watumie kifaa maalum cha usalama (kiti cha mtoto, kiti cha usalama wa mtoto au kiti cha mtoto chenye mgongo mrefu) ambacho kimeidhinishwa. Watoto wenye umri wa chini ya miaka 4 lazima wawe na kiti cha gari cha kuangalia nyuma wakiwa wanasafiri kwa gari.

Nchini Uswidi, magari ni ya mkono wa kulia, kumaanisha kwamba magari yote huendeshewa mkono wa kulia barabarani.

Soma maelezo zaidi kuhusu leseni za udereva ambazo zimeidhinishwa nchini Uswidi na jinsi ya kupata leseni ya udereva nchini Uswidi (kwa Kiingereza) External link, opens in new window.

Mwanamke ameketi kwenye tramu.

Picha: Shirika la Uhamiaji la Uswidi (Migrationsverket, The Swedish Migration Agency)/Björn Bjarnesjö

Ununuzi wa bidhaa

Nchini Uswidi, ununuzi mwingi wa chakula hufanyika katika maduka mbalimbali ukiwa nyumbani. Maduka madogo kwa kawaida huuza tu bidhaa za chakula, ilhali maduka makubwa pia huuza nguo, zana na vifaa vya kielektroniki.

Maduka ya bidhaa za chakula yanayouza vyakula kutoka mataifa mengine kwa kawaida hupatikana katika miji mikubwa kiasi na miji mikubwa. Katika miji mingi mikubwa, kuna vituo vyenye maduka ya kuuza vyakula, vifaa vya kielektroniki, nguo na viatu, lakini pia unaweza kupata, kwa mfano, wasusi, mikahawa na hoteli.

Mwanamume na mtoto wananunua bidhaa.

Picha: Plattform/Scandinav/imagebank.sweden.se

Mazingira na kutumia taka kutengeneza bidhaa mpya

Nchini Uswidi, kila mtu anatarajiwa kuchangia katika utunzaji wa mazingira na kuishi kwa njia ya kutunza mazingira kwa ajili ya kudumisha mazingira bora ya baadaye.

Ni kawaida kutumia mabaki ya vitu kutoka kwenye taka kutengeneza vitu vipya. Hii inajulikana kama kutumia taka kutengeneza bidhaa mpya. Makazi mengi yana vyumba vya kutupa taka ambapo taka huchujwa na kuwekwa katika vyombo au mapipa tofauti ya taka ambayo kisha huchukuliwa na lori la taka. Ni manispaa na mwenye nyumba ambao huhakikisha kwamba taka imekusanywa, lakini ni wakazi ambao wanapaswa kuchuja taka ipasavyo.

Kwa Waswidi, kutumia taka kutengeneza bidhaa mpya ni suala muhimu la utunzaji mazingira. Katika chumba cha kawaida cha kutupa taka utapata vyombo na mapipa ya taka ya chakula, glasi, karatasi, kadibodi, chuma, plastiki na vifaa vya kielektroniki. Ikiwa unaishi mahali ambapo hakuna chumba cha kawaida cha kutupa taka, unapaswa kubeba taka yako na uende uichujie katika vituo vya kutupa taka.

Nchini Uswidi, ni kawaida kwa vitu na bidhaa kutumiwa tena, k.m., kwa kununua nguo na vitu vya samani (viti, meza n.k) vya mtumba/vilivyotumika. Kuna maduka katika maeneo mengi ambapo unaweza kununua na pia kuuza bidhaa zilizotumika. Hii ni njia ya kuokoa pesa na pia inatunza mazingira.

Mwanamume na mtoto wanatumia taka kutengeneza bidhaa mpya.

Picha: Cecilia Lantz/imagebank.sweden.se

Wanyama na mazingira asili

Nchini Uswidi, ni kawaida kwenda matembezi katika mazingira asili kwa ajili ya shughuli mbalimbali. Kupitia haki ya ufikiaji wa umma, unaruhusiwa kutembea katika mazingira asili bila kibali chochote maalum. Kwa mfano, unaweza kutembea, kukimbia, kuendesha baiskeli, kuteleza kwenye barafu au kupiga kambi katika mazingira asili. Hata hivyo, hupaswi kukaa katika bustani la wenyewe au kutembea kwenye shamba lililolimwa. Hupaswi kuchafua au kuharibu mazingira asili, na hupaswi kudhuru au kusumbua wanyamapori wanaoishi huko.

Kuna sheria zinazolinda wanyama, kumaanisha kwamba wanyama wanapaswa kutunzwa vizuri na kulindwa kutokana na magonjwa na mateso. Wanyama wana sehemu muhimu katika maisha ya watu wengi. Kwa mfano, ni kawaida kuwa na mbwa au paka nyumbani na wanapaswa kutunzwa kama wanafamilia. Wanyama pia wana haki ya kuishi maisha mazuri bila kuumizwa kimwili au kiakili. Kwa hivyo unaweza kuadhibiwa kwa kumpiga au kumpiga teke mnyama.

Wanawake wawili wanatembea na mbwa na wanafanya mazoezi.

Picha: Lindsten & Nilsson/imagebank.sweden.se

Maswali ya kuzingatia

  • Unazungumza lugha ngapi? Je, unafikiri ujuzi wako wa lugha unaweza kukusaidia kujifunza Kiswidi?
  • Uswidi ina kiwango cha juu cha teknolojia. Umewahi kutumia zana dijitali na unafikiri utahitaji nini ili kujifunza kutumia huduma dijitali?

Last updated: